Huhitaji Taarifa Nyingi Kufanya Maamuzi Sahihi

Kutokujiamini na Kutegemea Maoni ya Wengine

MARA NYINGI tunapenda sana kuambiwa na watu wengine nini tunapaswa kufanya. Kutokujiamini kunatufanya tufikiri watu wengine shauri ya elimu yao, uzoefu wao, ujuzi wao, ndio wenye taarifa sahihi kuhusu maisha yetu. Tunachosahau, hata hivyo, ni kwamba wakati mwingine kutegemea sana maoni ya wengine kunaweza kukuingiza kwenye matatizo. Ukweli ni kwamba hakuna mtu anayeweza kukufahamu vizuri zaidi kuliko wewe mwenyewe. Tunasahau kuwa ufahamu ambao Mungu ametupa una nguvu kubwa ya kubadili maisha yetu ikiwa tutajua namna nzuri ya kuutumia. Huu ndio msingi wa Malcolm Gladwell kwenye kitabu chake cha ‘Blink”.

Nguvu ya Uelewa wa Haraka

Huwa unafanya nini unapotaka kufanya maamuzi? Unasubiri kulielewa jambo kwa asilimia 100? Gladwell anasimamia kuwa asilimia kubwa ya taarifa tunazozitumia kufikia maamuzi hazitusaidii. Ukiwa na asilimia kama 40 tu taarifa, unaweza kufanya maamuzi. Kwanza, ni ukweli kwamba kadri unavyongoja kupata taarifa zaidi, ndivyo unavyochelewa kuchukua hatua sahihi. Maamuzi yasiyosahihi yanayofanywa kwa wakati ni afadhali kuliko maamuzi sahihi yanayofanywa kwa wakati usiosahihi. Lakini pia, Gladwell anatudokeza suala muhimu. Taarifa za ziada unazopata zaidi ya ile asilimia 40 zinakufanya uchambua, upembue kupita kiasi na hatimaye unaweza kujikuta unachanganyikiwa usijue cha kufanya. Siri, kwa mujibu wa Gladwell ni kupata taarifa chache za msingi na kujizuia kuendelea kuchambua mafuriko ya taarifa ambazo wakati mwingine zinakuzuia kulielewa jambo husika.

Uwezo wa Kuhisi Usahihi wa Taarifa

Kadhalika, Gladwell anajenga hoja kwamba ufahamu wako unao uwezo mkubwa wa kuhisi usahihi wa taarifa mara tu unapokutana nazo. Unapokutana na mtu na kumtazama usoni, ukiwa makini, ndani ya dakika ya kwanza tu, unaweza kupata hisia ya nia yake ambayo mara nyingi huwa haionekani wazi. Wivu, chuki, hila na nia ovu aliyonayo mtu huonekana mapema ikiwa utakuwa makini. Usipuuze ‘machale’ haya ambayo wakati mwingine yanapingana na kile ambacho anachokisema.

Athari za Mazingira na Hisia Mbaya

Hata hivyo, pamoja na hulka hiyo tuliyoumbiwa, Gladwell anafikiri uwezo huu huzuiwa na mazingira fulani fulani kama vile kuzidiwa na mawazo, shinikizo kwenye ufahamu, kukosa amani na hata  sonona. Unapokuwa umekerwa na jambo, moyo wako umenyong’onyea, unajisikia kufedheheka, hasira zimekupanda, Gladwell anasema hapo huwa unakuwa umepoteza uwezo huu. Ufahamu wako katika mazingira haya hujielekeza kutafuta taarifa za kung’amua hatari ili uweze kuzitumia kujituliza, kukufanya urudi kwenye hali ya kawaida, ujione uko sahihi na hata kujitetea kwa kushambulia kile unachokiona kama kina hatari ndani yake. Ndio maana inashauriwa kwamba unapokuwa umekasirika, huna amani, umekata tamaa, huo sio wakati muafaka wa kufanya maamuzi. Ule uwezo ambao Mungu ametuumbia ndani yetu, unaotusaidia kupata taarifa muhimu kwa urahisi, unakuwa umekwamishwa. Jitahidi kupata muda wa kutulia, kumaliza hasira zako, kisha ufanye maamuzi ukiwa kwenye hali ya utulivu.

Imani Zinazoweza Kupotosha

Ukiacha hali hiyo ya ufahamu kuzidiwa na taarifa hasi, wakati mwingine ubongo wako unaweza kubeba na kuamini taarifa zisizosahihi na kuzing’ang’ania. Gladwell anaeleza kuwa taarifa hizo zinaweza kufukia uwezo wako wa asili wa kuhisia taarifa sahihi. Kuna mambo ufahamu wako umeyakusanya tangu ukiwa mdogo yanayoadhiri vile unavyoelewa mambo unayokutana nayo. Mfano, unaamini mtu mwenye elimu kubwa ya darasani, maana yake atakuwa na busara; mwanamke mrembo lazima atakuwa na tabia njema; mwanamume mwenye uwezo wa kifedha, anafaa kuwa mume. Imani kama hizi zinaweza kukupoteza kwa sababu busara za mtu hazina uhusiano na kiwango chake cha elimu. Tunao ma-Profesa wengi tu wanaoaminika kwenye maeneo yao ya taaluma, lakini hawana busara kwenye maisha ya kawaida. Tumeshuhudia wanawake wengi warembo wanaoshindwa kuishi na wanaume kwa sababu hawana tabia njema kinyume na matarajio ya wengi. Kadhalika, tunawafahamu wanaume wengi wenye uwezo mkubwa wa kifedha wanaokimbiliwa na wanawake lakini mwishowe wameishia kuwatesa wanawake kwa vitendo vya kikatili. Hiyo inamaana kuwa si kila tunachokiamini kinaweza kuwa kweli.

Kagua Upya Msimamo na Imani Zako

Kwa kuzingatia ukweli huo, Gladwell anashauri kukagua upya misimamo na imani ulizonazo kuhusu maisha, watu na matukio. Kuelewa kuwa wakati mwingine ufahamu wako unaamini vitu visivyo na ukweli utakusaidia kukataa hisia zinazotokana na misimamo uliyokuwa umeishikilia tangu zamani. Kadhalika, badala ya kuamini kirahisi taarifa, Gladwell anafikiri kukusanya taarifa zaidi itakusaidia. Usiruhusu misimamo yako iathiri namna unavyoyatazama mambo. Katika kila taarifa unayokutana nayo, fikiria ile asimilia 40 yenye taarifa za msingi na usiruhusu asilimia 60 ya taarifa zilizochanganyika na mambo unayoyaamini, taarifa hasi, inayoathiri maamuzi yako.

Pitio hili la kitabu limeandikwa na Christian Bwaya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa LEARNING Inspire® TANZANIA. Unaweza kuwasiliana naye kwa e-mail: bwaya@learninginspire.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *