Kujua Mengi Pekee Hakutoshi
Umewahi kumsikiliza mtu anayeonekana kujua vitu, mwenye maarifa ya kina lakini hakuvutii kumsikiliza? Umewahi kushangaa inakuwaje unaongea kitu cheny uzito unachoamini kitawasaidia wasikilizaji wako lakini hawaonekani kuvutiwa na hicho unachokisema? Ukweli ni kwamba kuzungumza ni zaidi ya kuwa na taarifa sahihi. Uzungumzaji ni una siri zake. Kitabu cha āTalk Like TEDā kilichoandikwa na Carmine Gallo kimechambua mazungumzo zaidi ya 500 kwenye jukwaa maarufu la TED Talks. Carmine amejaribu kuchambua vitu vinavyofanya hotuba zinazotolewa kwenye jukwaa la TED ziwasisimue wasikilizaji. Nukuu yake kubwa ni, āHatua ya kwanza ya kuwasisimua wasikilizaji wake, ni kuhakikisha wewe mwenyewe unasisimuka kwa kile unachokizungumza.ā TED ni kifupisho na maneno āTeknolojiaā, āElimuā na āMaendeleoā, kumaanisha kuwa wazungumzaji wanaokaribishwa kuzungumza kwenye tukwaa hilo hujikita kwenye maeneo hayo matatu. Unaweza kuangalia video za jukwaa hilo kwenye mtandao wa You Tube.
Sifa za Mzungumzaji
Kanuni ya kwanza ya ushawishi ina masuala matatu makubwa. Kwanza, sifa za mzungumzaji. Wasikilizaji wana tabia ya kujiuliza, wewe unayezungumza ni nani? Hicho unachokizungumza unakijua? Msikilizaji asipokuamini, huwezi kumgusa. Lazima kujitahidi kuhakikisha unazungumza masuala ambayo una hakika unayafahamu vyema kwa maana ya kuyasomea, una uzoefu nayo au ndiyo unayoyafanya. Pili, ushahidi. Mazungumzo yasiyoambatana na ushahidi wa takwimu, tafiti, uzoefu halisi wa watu, matumizi ya vyanzo halisi vya taarifa, hawezi kuwa na ushawishi mkubwa. Unapozungumza lazima ufanye marejeo kwenye vyanzo sahihi vya taarifa. Kanisani, rejea vifungu vya biblia. Msikitini, rejea msaafu. Kwenye kumbi za mikutano ya kitaalam, rejea takwimu na tafiti zilizokwisha kufanyika.
Kugusa Hisia za Wasikilizaji
Tatu na muhimu zaidi, Carmine anataja uwezo wako wa kugusa hisia za wasikilizaji wako. Usipojua namna ya kugusa mioyo ya watu unaongea nao, unaweza kushangaa una sifa zote, una takwimu na tafiti lazima hakuna mtu anapokea kile unachokisema. Ili kufanya hivyo, Carmine anashauri utumie masimulizi. Simulia tukio lako mwenyewe au la mtu mwingine linalofanana na kile unachokisema. Mara nyingi watu wanaposikia masimulizi ya maisha ya kawaida, inakuwa rahisi kuelewa kile unachokisema. Unaporejea masimulizi kama haya hoja yako inaeleweka kirahisi zaidi.
Matukio na Takwimu Zisizo za Kawaida
Somo la pili tunalojifunza kwenye kitabu hiki ni mbinu za kuhakikisha kuwa kile unachokisema kinakumbukwa kwa muda mrefu. Ili kufanya hivyo, mwandishi anapendekeza utumie matukio au takwimu zisizo za kawaida kukazia mazungumzo yako. Usiseme vitu vya kawaida ambavyo msikilizaji atavichukulia kirahisi rahisi. Simulia vitu vitakavyomfanya mtu ajiulize maswali kwa sababu unachokisema kinaonekana kuwa tofauti na kile anachokijua. Bill Gates anaonekana kujua mbinu hii vizuri. Wakati anazungumzia tatizo la malaria barani Afrika, aliwaachia mbu ukumbini wakawangāata wasikilizaji wake. Mbinu hii ilifanya mazungumzo yake yawe na nguvu kwa watu wale.
Sema Kitu Kipya au kwa Namna Mpya
Ukitaka watu wakumbuke kile unachokizungumza, sema kitu kipya. Hata kama si kipya kivile, kizungumze kwa namna mpya. Kwa mfano, watu wanafahamu kuwa kutokupata muda wa kukaa na watoto wao kuna athari katika malezi. Lakini ukiwaambia kwamba ikiwa watapata dakika 10 kila siku kukaa na watoto wao, watakuwa wameweza kukaa na watoto wao kwa muda wa mwezi mmoja watoto hao watakapofikia umri wa kuondoka nyumbani wakiwa na miaka 13. Lugha kama hii inasaidia mtu kutengeneza picha halisi ya kile kinachozungumzwa hata kama tayari alikuwa anakielewa kabla. Siku nyingine unapozungumza na watu, tumia masimulizi na takwimu kwa lugha rahisi kuwafanya watu wajenge picha ya kile unachowaeleza.
Zungumza kwa Muda Mfupi
Mbinu ya tatu ni kuhakikisha huzungumzi kwa muda mrefu. Hata jambo liwe zuri namna gani likirefishwa sana linakosa mvuto. Jukwaa la TED Talk lina kanuni ya wazungumzaji wao kuzungumza si zaidi ya dakika 18. Hata utafiti wako uwe na matokeo mengi namna gani, sheria ya TED ni kufupisha uongee kwa muda usiozidi dakika 18. Carmile anashauri usiongee muda mrefu kupitiliza. Tumia dakika chache lakini hakikisha unachoongea kinagusa mioyo ya watu kuliko kuzungumza muda mrefu kiasi cha kufanya kile unaachoongea kipuuzwe. Anza mazungumzo yako kwa kutumia masimulizi yanayohusiana na maisha ya kila siku. Tumia masimulizi hayo kujenga shauku ya watu kukusikiliza, kisha taratibu ingiza takwimu na nadharia zinazokazia kile ulichokisimulia. Kwa namna hii watu watatamani kukusikiliza.
Pangilia Hoja Chache na Rahisi
Pia usisahau kuwa ubongo wa mwanadamu hauwezi kusikiliza mambo mengi kwa wakati mmoja. Ndio maana tarakimu kama 196119641977 haziwezi kukaa ubongoni kirahisi mpaka ziweke kwa utaratibu mwepesi kueleweka mfano 1961, 1964, 1977. Siku zote unapoongea, usiwe na hoja nyingi kupita kiasi. Pangilia mambo yako uyasema kwa hoja tatu kubwa ukiweka na mifano. Hakuna sababu ya kuzungumzia mambo mengi yanayoweza kumchanganya msikilizaji. Sema mambo machache kwa lugha rahisi ili anayekusikiliza asipotee. Ikiwa unataka kutumia teknolojia ya uwasilishaji kwa āPowerpointā hakikisha āslideā zinakuwa na maneno machache. Badala ya kujaza maneno mengi, tafuta maneno machache muhimu yatakayokazia kile unachokisema. Kila inapowezekana, tumia michoro, picha na majedwali kutegemeana na aina ya mazungumzo yako. Kwa kufanya hivyo, unaweza kushangaa namna mazungumzo yako yatakavyopokelewa kirahisi.