Mambo ya Kufanya Uishi Vizuri na Watu

Epuka Ukosoaji na Hukumu

Maisha ni watu. Ukishindwa kuishi vizuri na watu mambo yako mengi hayataenda vizuri. Unaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kiakili, fedha na uwezo mwingine, lakini kama hujajifunza vizuri namna ya kuishi na watu, utakwama. Utashangaa unaweza kuwa na mawazo mazuri lakini yanakataliwa. Unakuwa na ushauri wa busara kwa mtu lakini yule unayetamani aupokee anaukataa kwa sababu tu hujajua namna ya kufikisha ujumbe kwa anayehusika. Kwa kutambua umuhimu wa kujua namna ya kuishi na watu, Dale Carnegie alindika kitabu maarufu cha, “How to Win Friends and Influence People.” Kitabu hiki kinatupa mwangaza wa namna  tunavyoweza kuishi vizuri na watu kwa kupendekeza mbinu kadhaa. Carnegie anaanza kitabu chake kwa kutufundisha mbinu za kuwafanya watu wavutwe kuwa na wewe. Kwanza, usiwe mtu mwepesi kukosoa, kuhukumu au kulalamika. Hata wakosoaji hawafurahii unapowakosoa kwa kukosoa kwa sababu kila mmoja angependa kuamini yuko sahihi. Unapomkosoa unamfanya atake kujitetea kwa minajili ya kuonesha kuwa yeye yuko sahihi na wewe umekosea. Ukosoaji  ni hatari kwa sababu unajeruhi hisia za mtu na kumfanya ajione amepungukiwa. Ile fahari tunayokuwa nayo kama binadamu inapotea pale unapokosolewa.

Onyesha Pongezi za Dhati

Kinyume chake mwandishi anatuada kujifunze kuona chema kwa watu na kutoa pongezi za dhati kwa chema kilichofanyika. Carnegie anasema kila mjinga anaweza kuona mapungufu na kuyazungumzia. Kila mtu hata yule asiye na busara anaweza kulalamika na kuwahukumu wengine. Lakini mwenye busara huonesha busara zake kwa vile anavyowatendea hata wale wasiostahili heshima. Mwenye busara huwaheshimu watu bila kujali nafasi zao kwa sababu anajua hakuna mtu asiyependa kutambuliwa. Carnegie anatoa mfano wa kukumbuka majina ya watu unapokutana nayo. Jina la mtu linabeba uthamani wake. Unapolitumia kwenye mazungumzo, unamfanya mwenzako ajisikie kuheshimiwa kwa kiwango cha juu.

Epuka Mabishano na Heshimu Mawazo ya Wengine

Lakini pia, Dale Carnegie anatufundisha namna ya kuongeza ushawishi unapokuwa na mazungumzo na mtu. Kwanza, usipende kubishana na watu bila sababu. Kila inapowezekana kwepa mabishano. Unapobishana na watu mara kwa mara lengo lako linakuwa kutaka kuonesha kuwa uko sahihi na wao wamekosea. Unapokuwa mtu wa kubishana sana unawaumiza watu wakati mwingine bila hata wewe kujua. Ili upunguze tabia ya kubishana na watu, heshimu mawazo ya watu wengine hata kama hukubaliani nayo. Lakini pia pale unapogundua umekosea kama binadamu, uungwana na kukiri makosa kwa kumaanisha. Kukiri makosa kunaonesha kuwa wewe ni mwaminifu na unapofanya hivyo unaongeza ushawishi wako.

Kuwa Msikilizaji Mzuri

Unapozungumza na watu, Carnegie anashauri usipende kutawala mazungumzo. Mwache mwenzako aongee. Usimkatishe katishe mwenzako kwa sababu tu unahisi unajua anataka kusema nini. Jifunze kuwa msikilizaji. Mfanye mzungumzaji ajione kuwa anajua. Mpe uhuru asimulie kile kilichoujaza moyo wake. Hata kama unafahamu ukweli, huna sababu ya kumfanya mwenzako ajione mjinga. Ingawa ni kweli kuna nyakati huwezi kukubaliana na anachofikiri mwenzako, siku zote, jitahidi kuvaa viatu vya mwenzako kujaribu kuyatazama mambo kwa macho yake. Jenga tabia ya kuthamini mawazo na matamanio ya mwenzako hata kama hukubaliani navyo. Ukifanya hivyo, itakuwa rahisi kwa mwenzako kukusikiliza. Siku zote msikilizaji mzuri huwa ana ushawishi mkubwa.

Kuwaelekeza Wengine kwa Busara

Ikiwa unafikiri una haja ya kumgeuza mwenzako mawazo, Dale Carnegie anashauri mbinu kadhaa. Kwanza, anza kwa kutambua thamani ya mawazo ya mwenzako. Usikimbile kueleza mawazo yako bila kuonesha kuelewa mwenzako naye ana kitu cha maana anachokifikiri. Pongeza kwa dhati yale unayokubaliana nayo kisha bainisha mapungufu unayoyaona kwa uangalifu bila kuumiza hisia zake. Hapa ndipo unapohitaji kuwa makini. Ili kubainisha mapungufu ya mwenzako, unaweza kuwa mjanga kwa kuzungumzia mapungufu yako mwenyewe kwanza. Toa mifano inayokuhusu bila kudanganya. Unapokuwa na ujasiri wa kuongelea kile kilichopungua kwako, unampa mwenzako ujasiri wa kukabiliana na mapungufu yake pia. Ikiwa unafikiri ni muhimu kumwelekeza mwenzako kwenye mapungufu yake, huna sababu ya kufanya hivyo moja kwa moja. Unaweza kuuliza swali linalomfanya mhusika ajitafakari zaidi. Kwa mfano, badala ya kumwambia mtu kuwa amekudanganya, unaweza kumkumbusha kile alichowahi kukwambia kabla kwa kumwuuliza alikuwa na maana gani. Swali zuri likiulizwa vizuri linatosha kumfanya mtu ajitathmini zaidi kuliko maneno ya moja kwa moja yanayoumiza moyo wake. Kadhalika, wakati mwingine mtu anaweza kukubaliana na wewe lakini asibadilike. Carnegie anashauri kutanguliza staha unapozungumzia udhaifu wa mwenzako. Usiongelee mapungufu yake kwa namna inayoshusha thamani yake kama binadamu. Huna sababu ya kumsimanga na kumwaibisha kwa sababu tu amekosea. Badala ya kumdhalilisha mtu mstahi. Mtunzie siri. Mtie moyo na kumfanya aamini kosa alilolifanya linaweza kurekebishwa. Unapofanya hivyo unamjengea hamasa ya mabadiliko inayoanzia ndani ya mtu. Uwezekano wa kubadilika unakuwa mkubwa zaidi.  

Pitio la kitabu hiki limeandikwa na Christian Bwaya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa LEARNING Inspire® TANZANIA.  Unaweza kuwasiliana naye kwa e-mail: bwaya@learninginspire.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *