Jifunze Tofauti za Wanaume na Mwanamke

PENGINE umewahi kujiuliza inakuwaje kila siku mnagombania suala hilo hilo na mwenzi wako? Kwa nini hamfikii muafaka wa jambo unaloamini ni rahisi kueleweka? Migogoro mingi katika mapenzi na ndoa inatokana na kushindwa kuelewa mahitaji ya jinsia tofauti. Mume anafikiri kile anachokihitaji yeye ndicho anachokihitaji mke wake. Mke naye anafikiri kile anachokihitaji yeye ndicho anachokihitaji mume wake. Matokeo yake kila mmoja anajikuta akipigania mahitaji yake na kusahau mahitaji ya mwenzake. John Gray kwenye kitabu chake cha “Men are from Mars, Women are from Venus: The Classic Guide to Understanding the Opposite Sex” anachambua tofauti hizi za kimaumbile akiamini kuwa uhusiano baina ya wanaume na wanawake unajengwa kwa kuzielewa na kuziheshimu tofauti zao za kimaumbile. Hapa ninakuletea tofauti tatu kubwa.

Tofauti ya Njia za Kutatua Matatizo

Kwanza, kuna tofauti kubwa ya njia wanazotumia wanaume na wanawake wanavyotatua matatizo yao. Kwa mujibu wa John Gray, wanaume wanapokuwa na jambo gumu, huhitaji muda zaidi kufikiri kuliko kuongea wakati wanawake wanahitaji kuzungumza zaidi. Kama uko makini na mwenzako unaweza kukubaliana na mwandishi kwamba mwanamke anapokuwa na kitu kinachomsumbua moyoni mwake, hutamani kupata mtu wa kumsikiliza amwelewe hata kama mazungumzo hayo hayatakuja na ufumbuzi wowote. Kwa mfano, mke anapokutana na kitu kinachomwuudhi kazini anaporudi nyumbani anatamani kumwambia mumewe ili amsikilize na kuonesha kumwelewa. Bahati mbaya ni kwamba wanaume wengi wanapoelezwa mambo na wake zao, wanafikiri wanaombwa majibu. Ingawa ni kweli kuna nyakati mwanamke hueleza jambo kama namna ya kutafuta ufumbuzi, lakini mara nyingi lengo huwa kusikilizwa. Mwanamume unapotoa majibu ya haraka haraka bila kusikiliza, unamwuumiza mwanamke. Tofauti na mwanamke, mwanamume anapokutana na changamoto, mara nyingi hapendi kuongea sana. Hata kama kwa kawaida ni mwongeaji, wakati huu anapokuwa na jambo linalomsumbua moyoni, mwanamume hugeuka kuwa mkimya akifikiri zaidi cha kufanya kuliko kuongea. Ukimya huu unaweza kutafsiriwa kama kiburi na mwanamke lakini kimaumbile unamsaidia mwanamume kujipanga ili anapoongea awe na ufumbuzi. Tunachojifunza hapa ni kwamba mwanamume anahitaji kupewa muda wa ‘kujificha kwenye mawazo yake’ badala ya kulazimishwa kuzungumza wakati mwanamke anahitaji kusikilizwa anapoongea badala ya kuambiwa cha kufanya.

Tofauti ya Tafsiri ya Mapenzi

Tofauti ya pili ni namna wanaume na wanawake wanavyotafsiri mapenzi. Mwanamke ana hitaji kubwa la kupendwa kwa kuambiwa na kwa kufanyiwa vitendo vya kimapenzi. Unapompenda kimya kimya unamfanya awe na wasiwasi. Hupata hisia kuwa hapendwi vya kutosha. Mwanamume anayeelewa hitaji hili la mpenzi wake atafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa mpenzi wake anasikia mara kwa mara kuwa anapendwa, analindwa, anathaminiwa kuliko wanawake wengine, na zaidi ya yote ni kipaumbele cha maisha ya mume wake. Lakini mwanamume, tofauti na mwanamke, anatafsiri kupendwa kwa kuheshimiwa na kukubalika kwa uwezo alionao. Unapomfanya mwanamume ajione amekusaidia, amekuwa shujaa wa maisha yako, ametimiza wajibu wake kwako, unamfanya awe na nguvu za kukupenda zaidi. Kwa hiyo kama mwanamke jifunze kumwonesha mpenzi wako kuwa unamwamini, unauelewa uwezo wake kwa kutambua juhudi anazofanya, kwa kumwomba akusaidie na hata kumshukuru kwa kazi nzuri anayofanya kwa faida ya familia. Moja wapo ya sababu zinazowafanya wanaume wengi kupotelea kwenye michepuko ni ule uwezo wa wasichana ‘wezi’ kutambua uwezo wao na kuwaheshimu. Fanya hivyo nyumbani utaona mwanamume anavyoitikia kwa kukupenda zaidi.

Tofauti ya Matumizi ya Lugha

Tofauti ya tatu ni matumizi ya lugha. John Gray anasema wanawake hutumia maneno kuelezea hisia zao zilizojificha. Ili kumwelewa mwanamke unahitaji jicho la tatu. Kwa mfano, mwanamke anaposema, ‘Hujawahi kuninunulia kitenge!’ hamaanishi ‘hujawahi.’ Neno hujawahi ni namna ya kueleza tu hisia zake kwamba muda mrefu umepita hujamletea zawadi. Usipokuwa mwangalifu, unaweza kuanza kubishana hapo kuonesha kuwa mpenzi wako hana shukrani lakini ukweli wa mambo anajaribu kukukumbusha matamanio yake ambayo huenda umeyasahau. Tunachojifunza hapa ni kwamba kama mwanamume, usiishie kusikiliza neno lililotumika. Sikiliza neno hilo linabeba ujumbe gani. Tofauti na wanawake, wanaume hutumia maneno ya moja kwa moja ambayo wakati mwingine hayana hisia zilizojificha ndani yake. Kwa mfano, mume anamwambia mke wake, “Umenichosha!” Hapa mwanamke anaweza kuumia sana kwa kuamini mwanamume hana tena mpango na yeye. Lakini ukweli ni kwamba kwa mwanamume, “Umenichosha” inamaana kile alichokifanya mwanamke kwa wakati huo. Mwanamke akiweka hisia kwenye neno hilo, anaweza kuumia sana lakini kumbe sicho alichomaanisha mwanamume. Tunachojifunza hapa ni kwamba  kama mwanamke usifikiri sana kile unachokisikia kwa mpenzi wako. Kile alichokwambia mara nyingi huwakilisha vile anavyojisikia wakati huo.

Matarajio na Mahitaji Tofauti ya Wanaume na Wanawake

Kwa ujumla, mwandishi anajenga hoja kwamba wanaume na wanawake wanafikiri tofauti. Matarajio ya mwanamke ni tofauti na matarajio ya mwanamume. Kile ambacho mwanamume anakiona ni muhimu sio lazima kiwe muhimu kwa uzito ule ule kwa  mwanamke. Ikiwa na wewe ni miongoni mwa watu wasio na uhakika na mahitaji ya wenzi wao, kitabu hiki kinaweza kukufaa.  Ukipata uelewa wa namna mpenzi wako alivyo tofauti na wewe, ukaelewa namna uelewa wako kuhusu mahitaji yake ulivyo tofauti na uhalisia, matarajio yako kwake yanavyobadilika. Maarifa haya yatabadilisha uhusiano wenu na kutatua migogoro mingi isiyo ya lazima inayotokana na kukosekana kwa uelewa wa mwenzako.

Pitio la kitabu hiki limeandikwa na Christian Bwaya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa LEARNING Inspire® TANZANIA.  Unaweza kuwasiliana naye kwa e-mail: bwaya@learninginspire.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *