Siri ya Makampuni Yanayofanya Vizuri Sokoni

Changamoto za Makampuni Mengi Sokoni

MAKAMPUNI mengi hayafanyi vizuri kwenye biashara. Takwimu zinasema katika makampuni 10 yanayoanzishwa kila mwaka, makampuni zaidi ya nane hufa ndani ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa. Pamoja na sababu nyingine, changamoto kubwa ni namna ya kukabiliana na ushindani mkubwa kwenye soko, ushindani unaosababisha kufa kwa makampuni mengi na mengine mengi kujiendesha kwa hasara kwa miaka mingi. Ingawa ni kweli makampuni yanayopotea kwenye soko ni mengi, bado kuna ukweli kwamba yapo makampuni makubwa ambayo, pamoja na changamoto za hapa na pale, yameendelea kutawala masoko ya bidhaa na huduma wanazotoa. Siri ni nini? Kwa nini makampuni mengine yafe wakati mengine yakiendelea kufanya vizuri?

Kiwango cha Kushindwa kwa Makampuni Mpya

Kitabu cha ‘Good to Great’ kilichoandikwa na Jim Collins, kinajaribu kueleza hatua ambazo kampuni zilizokuwa za kawaida kabisa zinaweza kuchukua ili kuongeza ushindani wake vyema dhidi ya washindani. Kitabu hiki si hadithi za kusadikika, bali ni matokeo ya uchambuzi wa kina uliofanywa kwa kutumia makampuni 28 katika kipindi cha zaidi ya miaka 30, ambayo hatimaye yaliweza kubadili mifumo yake mibovu ya utendaji na kupata mafanikio makubwa.

Hatua za Mafanikio kwa Makampuni ya Kawaida

Pamoja na mengi anayoyabainisha Jim Collins kwenye kitabu chake, mambo matatu makubwa yanaonekana huchangia mafanikio ya kampuni yoyote. Moja, kutafuta na kuulinda upekee wa kampuni. Simba hawezi kuwa mfalme wa mwitu, kama hana uwezo wa kipekee wa kupambana na wanyama wengine wote. Fisi, tembo, swala, nyoka wanaweza kuja na mbinu za kupambana naye, lakini ule upekee wake utamfanya aendelee kuwa juu ya wote.

Umuhimu wa Kutafuta na Kulinda Upekee wa Kampuni

Huwezi kuwa kampuni kubwa yenye mafanikio kama hujajua upekee wako, upekee utakaokufanya uendelee kushindana na washindani wako kwa miaka mingi ijayo. Swali, hata hivyo, ni kwamba unaujuaje upekee wako? Collins anakupa maswali matatu. Mosi, jiulize, kitu gani unaweza kukifanya kwa ubora zaidi kuliko mtu mwingine yeyote duniani? Pili, vitu gani mnaweza kuvifanya kwa namna mnayoifuarahia zaidi? Tatu, viashiria gani vya kiuchimi vinavyoweza kuongoza maamuzi ya utendaji wenu? Ingawa maswali haya yanaweza kuonekana kuwa rahisi, Jim Collins anasema, kwa kawaida, inachukua zaidi ya miaka minne kwa makampuni yanayofanya vizuri zaidi kutafakari kwa kina kuja na majibu sahihi ya maswali hayo.

Maswali ya Collins kwa Upekee wa Kampuni

Suala jingine analolizungumzia Jim Collins ni umuhimu wa matumizi ya teknolojia. Dunia inakwenda kasi sana. Kila siku zinagunduliwa teknolojia mpya za kurahisisha utendaji wa kazi. Mitandao kama WhatsApp, Facebook, Twitter, Instagram haina miaka kumi tangu ijipatie umaarufu lakini imetawala maisha ya watu. Kuna watu wengi ambao hawawezi kukaa mbali na mitandao hii ya kijamii kwa zaidi ya robo saa. Lakini, je kila kampuni inaihitaji mitandao hii? Kwamba mitandao hii ina umaarufu hiyo haimaanishi ina umuhimu kwa kila kampuni. Collins anapendekeza kutumia teknolojia inayorahisisha shughuli za kampuni yako katika mazingira ambayo teknolojia hiyo inaendana na dhima kuu ya shughuli za kampuni yako.

Matumizi ya Teknolojia katika Makampuni

Katika kitabu chake, Collins anatoa mfano wa Walgreens iliyopata anguko la asilimia 40 ya hisa kwa uamuzi wake wa kukaa mbali na matumizi ya mtandao mwanzoni. Uamuzi huo, mwanzoni. uliwafanya washindani wake wapate nguvu. Hata hivyo, wakati huo huo, Walgreens walifanya uchambuzi wa kina kujua namna gani wanaweza kujiingiza kwenye biashara ya mtandao kukuza dhima yao ya kuwa kampuni kubwa zaidi ya kuuza madawa. Hatimaye waliweza kuja na mbinu bora zaidi ya kumpa mteja maelezo ya dawa kwa kutumia mtandao. Ugunduzi huo uliimarisha zaidi shughuli zao. Tunachojifunza hapa, usiwe mwepesi kurukia teknolojia. Fikiri kwa makini namna teknolojia hiyo inavyoweza kuimarisha shughuli zako.

Mfano wa Walgreens na Matumizi ya Mtandao

Somo la tatu, na kubwa, ni kwamba katika biashara ni muhimu kukabiliana na ukweli kwa wakati. Makampuni yanayofanya vizuri, kwa mujibu wa Jim Collins, yana tabia ya kuukubali ukweli mchungu mapema na kuchukua hatua za kuufanyia ukweli mapema. Makampuni haya hayafanyi kama afanyavyo mbuni anayejifariji kwa kuficha kichwa chake mchangani wakati mwili wote uko nje. Lakini pia, hunyanyui mikono juu ishara kuwa umekata tamaa. Unapoona dalili mbaya katika biashara, labda mauzo yamepungua kwa mfano, chukua hatua haraka. Usitumie uzoefu wako wa zamani kujifariji kuwa mambo yanaweza kubadilika. Unapoona sera za serikali zinabadilika tofauti na ilivyozoeleka, una kazi ya kujichunguza na kuona namna gani mabadiliko hayo yanaweza kuathiri utendaji wa shughuli zenu na hivyo kuchukua hatua kwa wakati. Usipofanya hivyo unajiweka kwenye hatari ya kujikuta unafunga biashara. Kwa upande mwingine, kuchukua hatua kunategemea kiwango cha ujasiri ulichonacho. Mambo yanabobadilika, usikimbilie kulalamika na kusubiri kupotea kwenye biashara. Lazima kuchukua hatua kwa ujasiri ukijua kuwa kufa kwa kampuni yako kunaweza kuwaathiri wengine lakini mhusika mkuu ni wewe.

Umuhimu wa Kukabiliana na Ukweli kwa Wakati

Kitabu hiki kimetumia matokeo ya utafiti wa kina ambao, kama nilivyotangulia kueleza, umehusisha makampuni mengi. Ikiwa wewe ni mfanyabiashara, mkuu wa kampuni au taasisi inayofanya aina yoyote ya biashara, kitabu hiki kinakufaa. Kadhalika, kwa viongozi wa taasisi zinazotoa huduma zinazohitaji ubunifu wa hali ya juu kujiimarisha kwenye soko la ushindani, kitabu  hiki kinaweza kuwafaa.

Pitio la kitabu hiki limeandikwa na Christian Bwaya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa LEARNING Inspire® TANZANIA. Unaweza kuwasiliana naye kwa e-mail: bwaya@learninginspire.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *