Robert Greene Anavyoichambua Hulka ya Binadamu

Umuhimu wa Kuelewa Hulka za Binadamu

Umewahi kujiuliza kwa nini wakati mwingine kuna vitu ungependa kuvifanya na unaelewa kabisa umuhimu wake lakini unashangaa huwezi kuvifanya? Kwa nini wakati mwingine unarudia kufanya maamuzi yale yale yaliyowahi kukuletea hasara? Hivi inakuwaje, kwa mfano, unajikuta unachumbia watu wenye tabia zile zile usizozipenda? Mambo yanaanza vizuri lakini baadae, unakuja kugundua umekutana na mtu mwenye tabia zile zile ulizozikimbia kwa mchumba wako wa mwanzo. Kurasa 624 za kitabu cha The Laws of Human Nature kilichoandikwa na Robert Green zinakupa mwangaza wa majibu ya maswali yanayofanana na hayo. Lengo la kitabu hiki, kwa maoni yangu, ni kumsaidia msomaji kuwaelewa watu wengine vizuri zaidi na hivyo kujikinga na watu wenye hulka ya kuwaumiza wengine. Lakini pia kitabu hiki kinakusaidia kujielewa zaidi, kujua hulka zetu kama binadamu kwa maana ya kuelewa kwa nini tunafanya yale tunayofanya.

Sheria ya Mihemko

Katika sheria 18 zinazochambuliwa kwenye kitabu hiki, hapa ninakuletea baadhi ya sheria hizo kukusaidia kujenga shauku ya kukitafuta na kukisoma kitabu hiki. Sheria ya kwanza inaitwa sheria ya mihemko. Robert Green anaeleza kwamba ingawa mara nyingi huwa tunapenda kujichukulia kama watu tunaofikiri sana kutumia ufahamu wetu kufanya maamuzi, ukweli ni kwamba mara nyingi tunaendeshwa mihemko. Tunapandwa na hasira bila sababu za msingi, tunawachukia watu wanaotusema vibaya, tunafanya manunuzi yasiyo ya lazima, tunachukua mikopo tusiyoihitaji, kwa sababu tu ya mihemko. Mwandishi anatuasa kujikagua na kujifunza namna ya kujizuia na kujipa muda wa kufahamu kwa nini tunataka kile tunachokitaka. Mafanikio yanategemea uwezo wetu wa kuelewa mihemko hii na kuidhibiti.

Sheria ya Ubinafsi

Sheria ya pili inaitwa sheria ya ubinafsi. Mwandishi anatueleza kwamba tangu enzi na enzi mwanadamu amekuwa na historia ya kuwa mtu mbabe, mbinafsi anayejiangalia mwenyewe. Ukiangalia matukio kama rushwa, ufisadi, uhalifu, mapigano baina ya watu, makabila, makundi ya kijamii, nchi na nchi, kilichowazi ni kwamba mitafaruku inachangizwa sana na ubinafsi wa watu wanaotaka kuwatumia wenzao kwa manufaa binafsi. Hulka hii haiwezi kutuletea maendeleo kama watu binafsi na jamii. Tunahitaji kujifunza kinyume chake kwa kuwa watu wanaojali wenzao, wanaoelewa mahitaji ya wenzao, na waliotayari kutafuta muafaka na wale wanaopingana nao. Kanuni hii inaweza kutusaidia kwenye familia, kazini, kwenye jamii na hata kwenye siasa za kitaifa.

Sheria ya Maigizo

Sheria ya tatu inaitwa sheria ya maigizo. Mwandishi anatueleza kwamba binadamu ana hulka ya kuigiza wema asiokuwanao. Tabasamu wakati mwingine huficha chuki iliyoufanga funga moyo. Kicheko kinaweza kuficha uadui na wivu alionao mtu. Matendo ya hisani yanaweza kuficha ubinafsi wa kuwatumia watu kujijengea sifa binafsi. Mwandishi anaelekeza namna tunavyoweza kutambua unafiki wa watu kwa kuelewa lugha ya mwili. Unapoelewa maigizo kwenye nyuso za watu inakusaidia kuchukua hatua mapema kabla hujaingizwa kwenye ‘mkenge’.

Sheria ya Kujihami

Sheria nyingine inaitwa sheria ya kujihami. Robert Green anatumia matukio ya kihistoria kutueleza kwamba binadamu siku zote ni mtu wa kujitetea. Penye makosa lazima atafute mtu wa kubeba lawama zake kwa sababu kukubali makosa kunachukuliwa kama udhaifu. Mwandishi anatufundisha namna nzuri ya kutumia hulka hii katika maisha. Badala ya kuwalaumu watu, kwa mfano, jifunze kukubali makosa yako. Badala ya kuwakumbusha watu mema uliyowahi kuwatendea, wakumbushe mema waliyowahi kukutendea wewe. Unapofanya hivi, unamfanya mtu akose nguvu ya kupambana na wewe na hivyo inakuwa rahisi kukubaliana na kile unachotaka akielewe.

Sheria ya Kuficha Uovu

Sheria nyingine inaitwa sheria ya ‘kuficha uovu.’ Robert Green anatuambia kwamba kila mtu ana upande mchafu asiopenda ufahamike. Usione watu wamevaa mavazi meupe yaliyotiwa nakshi ya alama za kidini ukaamini ni watakatifu. Watu wana mambo mengi wanayoyaficha. Ukiwafahamu unaweza kukata tamaa. Hata wewe unayetafuta kujua ubaya wa mtu una mambo yako usiyopenda yafahamike. Unajitahidi kuonekana ni mtu mstaarabu, mwenye busara, mcha Mungu lakini unajua ‘aibu’ yako imejifivha wapi. Green anatukaribisha kuufahamu na kuubali upande wa pili wa maisha yetu na kuutumia kwa manufaa.

Sheria ya Husda

Sheria ya 10 inaitwa sheria ya husda. Green anatumia mifano ya historia kutueleza namna mwanadamu amekuwa mtu mwenye hulka ya kushindana na wengine, kutamani kuwa bora kuliko wengine, kuwaona wenye mafanikio kama maadui, na tabia nyingine kama hizo.  Green anaeleza kwamba husda ni namna ya kudhihirisha hisia zetu za uduni. Tunapokuwa watu wa kuwalaumu wengine, kuwanyooshea vidole wengine, maana yake tunakubali kwamba ndani yetu kuna udhaifu tusiotaka kuukubali. Tunahitaji kujifunza kwamba hata hao tunaowaonea husda nao wana mapungufu yao. Hakuna sababu ya kujilinganisha na watu kwa sababu kila mtu ana namna yake ya kufanikiwa.

4 Comments

  1. Nimependa summary kitabu hicho
    Samahani nawez pata kitabu kilichotafsiriwa

    1. Habari za leo Anord, samahani ila hatuna kitabu cha ‘The Laws of Human Nature’ kilichotafsiriwa

  2. Ujumbe mzuri,ninashauku ya kuendelea kusoma Makala mbalimbali.

    1. Asante sana Yared, kuna makala mapya kwenye blog page yetu. Karibu sana na kumbuka kushare kwa ndugu na marafiki

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *