Ukiweza Kumsikiliza Mtu, Unaweza Kumshawishi

Ukiweza Kumsikiliza Mtu, Unaweza Kumshawishi

KWENYE kundi letu la WhatsApp la wasomaji wa vitabu, tumekuwa na kawaida ya kuchagua kitabu kimoja wapo na kukisoma kwa pamoja. Baada ya kusoma sehemu husika kwa juma, majadiliano makali hufuata yakiongozwa na mwenyekiti wa mjadala kwa juma husika. Katika majadiliano hayo, kwa kawaida, wasomaji hucheua kile walichokipata kitabuni na kujaribu kukihusisha na maisha yao ya kila siku.

Kitabu “Just Listen” cha Mark Goulston

Katika vitabu tulivyowahi kuvisoma na vikanigusa ni kitabu kiitwacho “Just Listen: Discover the Secret to Getting Through to Absolutely Anyone” kilichoandikwa na Mark Goulston. Binafsi kitabu hiki kimenisaidia kupanua uelewa wangu kuhusu namna bora ya kuwasiliana na watu. Goulston anapendekeza mbinu kadhaa zinazoweza kumsaidia yeyote kutengeneza mazingira ya kuelewana na watu.

Jinsi ya Kujenga Ushawishi kwa Kusikiliza

Somo la kwanza nilililojifunza ni namna bora ya kujenga ushawishi kwa mtu. Sote, kwa nyakati tofauti, tunapenda kuwashawishi watu wakubaliane na mitazamo na maoni yetu. Tunahitaji ushawishi katika biashara, kazini, mahusiano, siasa na maeneo mengine. Katika nyakati tunazofikiri tunahitaji kubadilisha mitazamo ya wengine, ipo haja ya kujua kuwa binadamu habadiliki kirahisi rahisi kwa sababu kwa kawaida, ana hulka ya kusimamia kile anachokiamini. Unawezaje kumshawishi mtu kukubaliana na mtazamo wako? Mwandishi anatupa mbinu ya kusikiliza.

Mbinu ya Kuakisi Hisia za Mwingine

Kusikiliza, kwa mujibu wa Goulston, ni kuakisi kile anachokisema mtu hii ikiwa na maana ya kusema kwa sauti kile unachoamini mwenzako ndicho anachokifikiria. Mwandishi anatumia mfano wa mtu aliyekuwa anakaribia kujiua kwa kujipiga risasi kichwani hadharani. Polisi waliwasili kwenye eneo hilo la tukio kujaribu kumnusuru. Kwa kuzingatia kuwa jamaa huyu aliyekata tamaa na maisha alikuwa kashika silaha, ilibidi kufanya mazungumzo naye. Polisi walitumia muda mwingi kumweleza kwa nini kujiua ni kinyume cha sheria lakini yule bwana alibaki kimya.

Uhalisia na Kujionesha Udhaifu

Lakini baadae alikuja afisa mwingine aliyetumia mbinu tofauti. Yeye alijitahidi kuonesha anaelewa kile kinachomsibu jamaa huyu. Maneno aliyomwambia ni kama haya, “Najua unaamini hakuna mtu mwingine anayeweza kukusaidia kwa sababu hawakuelewi na kila ulichojaribu kukifanya hakijawezekana, si ndio?”Jamaa aliitikia kuonesha kuwa kilichosomwa ni sahihi.

Umuhimu wa Shukrani ya Dhati

“Najua unaamini hakuna mtu anayeelewa kuwa kila siku unapoamka huoni njia, na kila unachojaribu kukifanya hakileti matokeo, si ndio?” Maneno kama haya yalimwingia huyu bwana mithili ya mshale na kumfanya ajisikie kueleweka. Taratibu hasira ikaanza kumtoka, akaanza kujibu maswali kwa maelezo marefu ya kujieleza kwa nini amefikia uamuzi huo. Mwuulizaji alibaki kurudia rudia tu kile alichokuwa anakisikia kuonesha kuwa kweli anasikiliza na kuelewa kinachosemwa. Baada ya muda, yule bwana alitupa silaha na kuahirisha jaribio lake.

Jinsi ya Kuonesha Shukrani kwa Usahihi

Kwanza, lazima ielekezwe kwenye suala mahsusi alilolifanya mtu. Mfano, “Asante sana mke wangu kwa kukaa na watoto muda wote nilipokuwa kazini.” Pili, shukrani lazima itambue jitihada za mtu. Mfano, “Natambua wewe ni mtu mwenye mambo mengi na kwa kweli hukuwa na sababu ya kuacha shughuli zako na kuja kunitembelea. Umejali na kuamua kutoa muda wako kwa ajili yangu.” Tatu, shukrani lazima ionesha namna kile kilichofanywa kilivyokusaidia. Mfano, “Mara nyingi ninarudi nyumbani nikiwa hoi kwa uchovu wa kazi. Uliponisaidia kusafisha vyombo nimepata muda wa kumpumzika kidogo. Shukrani sana.” Haya ndiyo mambo makubwa niliyojifunza kwenye kitabu hiki. Napendekeza usome kitabu hiki kuimarisha uhusiano wako na watu kwenye maeneo mbalimbali.

Pitio hili la kitabu limeandikwa na Christian Bwaya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa LEARNING Inspire® TANZANIA.  Unaweza kuwasiliana naye kwa e-mail: bwaya@learninginspire.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *