Maamuzi ya Ajabu ya Julian Mantle: Kutoka Wakili Maarufu hadi Kasisi
UNGESIKIA mtu ameuza kila alichonacho, nyumba, magari, biashara zake, mashamba, akaacha kazi na starehe za mjini akaamua kurudi kijijini, ungemwelewaje? Unafuatilia maisha yake kule alikokwenda unashangaa hana cha maana anachofanya. Wengi wetu tungefikiri huyu lazima atakuwa amechanyikiwa. Mtu mwenye akili timamu hawezi kufanya maamuzi ya namna hii. Ndivyo kinavyoanza kitabu cha “The Monk Who Sold His Ferrari” kilichoandikwa na Robin S. Sharma. Mhusika mkuu wa kitabu hiki ni Julian Mantle mwanasheria aliyeamua kuuza gari lake la thamani aina ya Ferrari na kuamua kuwa kasisi. Julian Mantle, mhitimu wa Shule Kuu ya Sheria Havard alijipatia umaarufu mkubwa kama wakili machachari nchini Marekani kwa uwezo wake mkubwa wa kuwatetea wateja wao na kushinda mashauri yao mahakamani. Kazi yake ilimfanya Julian Mantle awe na kila kitu ambacho mwanadamu angetamani kuwa nacho. Lakini pamoja na mafanikio hayo, Mantle hakuwa na amani. Kazi zilikuwa nyingi kuliko uwezo wake, na karibu kila siku alikuwa na shauri jipya la kushughulikia mahakamani. Wingi wa kazi ukaibua tatizo la msongo wa mawazo. Siku moja akiwa mahakamani, Julian alipatwa na kiharusi akashindwa kuendelea na kazi. Tukio hilo lilibadili kabisa maisha yake. Baada ya hapo hakuwasiliana tena na wateja wake. Tetesi zikaanza kuenea mjini kuwa Julian aliamua kwenda India kuanza maisha mapya -jambo ambalo lilikuwa kweli. Kabla hajaondoka, Julian aliuza jumba lake na gari lake la kifahari. Moyoni mwake aliazimia kuwa maisha ni zaidi ya mali na vitu vinavyoonekana. Baada ya miaka mitatu, Julian alirudi mjini kimya kimya. Julian alipomtembelea rafiki yake ofisini, mwonekano wake ulikuwa tofauti. Uso wake angavu ulipambwa na tabasamu pana la ki-Buddha. Julian alikuwa amejifunza mfumo mpya wa maisha. Kumbe akiwa nchini India kwa miaka hiyo mitatu, Julian alisafiri maeneo mbalimbali na kukutana na watawa wa dini ya ki-Buddha waliomfundisha maisha mengine ya kiroho yaliyombadilisha kuwa mtu mwenye utoshelevu zaidi.
Mafunzo ya Julian kutoka kwa Yogi Raman: Kanuni Saba za Maisha ya Utoshelevu
Mwandishi Robin anatumia simulizi hili linatufundisha kanuni saba za maisha yenye utoshelevu. Kanuni hizi Julian alijifunza kwa Yogi Raman, mmoja wapo wa watawa wa ki-Buddha aliokutana nao nchini India. Katika mazungumzo yake ya mara kwa mara na Raman yaliyolenga kujifunza maana hasa ya maisha na namna ya kuishi maisha yenye utoshelevu, Julian akajikuta akigeuka kuwa mwanafunzi wa mafundisho yaliyoitwa Maisha ya ki-Sivana yenye nguzo kuu saba.
Nguzo ya Kwanza: Kudhibiti Mawazo kwa Maisha Yenye Amani na Utoshelevu
Nguzo ya kwanza inasema, utoshelevu katika maisha unaanza na uwezo wa mtu kudhibiti mawazo yake. Kwa kawaida maisha hutujaza fahamu zetu na mawazo hasi, hofu na wasiwasi. Tangu tunaamka asubuhi mpaka tunapokwenda kulala, fahamu zetu zinameza kila aina ya uchafu unaogeuka kuwa usumbufu kwenye mawazo yetu. Ingawa hatuoni athari hiyo kwa urahisi, takataka tunazoingiza kwenye fahamu zetu zinajenga mfumo mwingine wa maisha yetu. Julian alijifunza mfumo mpya wa maisha unaoanza na kuingiza mawazo ya amani kwenye fahamu zake. Somo la kwanza alilojifunza ni kwamba ili kuwa na amani, kuishi maisha yenye utoshelevu, ni muhimu kuruhusu mawazo yaliyojaa amani yatawale fahamu zake. Swali, hata hivyo, tunawezaje kufundisha fahamu zetu nini cha kufikiri na nini cha kuachana nacho? Siri ni rahisi. Sote tuna uwezo wa kuchagua aina ya mawazo yetu ikiwa tutajizoesha. Hatua ya kwanza ni kujifunza kuzingatia. Jenga tabia ya kwenda mahali palipotulia na kutuliza ufahamu wako. Katika hali ya utulivu, unaamua kipi ukiache kitawale ufahamu wako na kipi unakizuia. Ukifanya hivi kila siku, ukajenga mazoea ya kupata mahali pa utulivu, zoezi la kuiamrisha akili yako iwaze nini litakuwa rahisi.
Nguzo ya Pili: Kugundua Kusudi la Maisha na Kuishi Utume Wako
Nguzo ya pili ya maisha ya utoshelevu ni kujua unaishi kwa sababu gani. Maisha yako yanalenga nini? Ma-Buddha walimshangaza Julian Mantle kwa vile walivyoonekana kuwa watu wasiopoteza muda. Kila walichokifanya kilionekana kukamilisha lengo kuu. Hawakupoteza muda bila sababu. Julian alijifunza neno ‘dharma’ lenye maana ya ‘kusudi la maisha.’ Neno hili lina asili yake kwenye imani ya kale, kwamba kila binadamu ana utume wa kuukamilisha. Ndio kusema, utoshelevu anaoupata mwanadamu unategemea namna gani anaweza kuuishi utume huo. Tunapozungumza utume, kusudi la maisha, swali mara zote ni, “Unawezaje kujua umezaliwa kufanya kitu gani?” Swali hili halikujibiwa moja kwa moja na mafundisho ya Raman. Hata hivyo, inavyoonekana uwezo wa kuwa na malengo bayana katika maisha ndio hatua ya kwanza kabisa ya kutanabaisha kusudi la maisha. Changamoto, hata hivyo, ni kuwa na malengo ambayo wakati mwingine hatuyatekelezi. Raman anapendekeza hatua tano. Kwanza, kujenga taswira ya kile tunachotaka kitokee. Kama lengo lako ni kuwa na kampuni kubwa ya biashara, lazima uanze kwanza kuiona kampuni hiyo kabla hata hujaianzisha. Lakini pili, Raman anasema lazima kujiwekea aina fulani ya msongo utakaokusukuma kutekeleza unachokitaka. Kwa mfano, badala ya kukaa kimya na ndoto zako, waambie watu kile unachotaka kufanya. Kisha, jiwekee ukomo. Malengo yasiyo na muda unaoeleweka wa kuyatekeleza, hufa kabla hayajaanza. Nne, ni kutokusubiri. Ukishapanga jambo anza utekelezaji kwa siku 21 mfululizo usiahirishe. Ukiweza kufanya hivyo, hiyo itageuka kuwa tabia.
Nguzo ya Tatu: Uendelevu na Kujiboresha Kila Siku kwa Bidii
Katika nguzo ya tatu, mwandishi anajenga hoja katika ukweli kwamba kufikia kimo cha utume wa maisha yako si suala la siku moja. Lazima kutia bidii ili kuendelea kujiumba kuwa mtu bora. Kanuni hii inaitwa uendelevu na inahitaji hatua kadhaa. Kwanza, ni kujenga tabia ya kuwa na muda wa ukimya kukuruhusu kutuliza akili yako. Unapokuwa na utulivu, inakuwa rahisi kuachilia ubunifu ulio ndani yako. Hatua nyingine ni kujilisha maarifa. Huwezi kuliishi kusudi lako bila kujifunza mambo mapya. Jenga tabia ya kusisimua ufahamu wako kwa kujisomea na kujifunza mambo ambayo pengine hujawahi kuyafahamu. Lakini hiyo haitoshi, lazima kupata muda wa kujitathmini mithili ya mtu anayemtazama mtu mwingine na kujihoji. Je, uko kwenye mstari sahihi? Kuna ambacho ungeweza kukifanya tofauti? Kingine, ni kujisemea maneno unayotaka yatokee. Maneno yana nguvu ya uumbaji. Usisubiri mtu mwingine akuhamasishe. Jihamasishe mwenyewe kwa maneno sahihi. Lakini pia, katika kujenga uendelevu ishi maisha rahisi. Urahisi wa maisha unaanza na hatua ya kujua wapi pa kuelekeza vipaumbele vyako. Mtu anayejua afanye nini na muda wake mara anapoamka, hawezi kuwa na mambo mengi yasiyomsaidia kufikia malengo yake.
Nguzo ya Nne: Kuishi Maisha ya Nidhamu na Kudhibiti Muda
Nguzo ya nne ni kuishi maisha ya nidhamu. Katika mazungumzo yake na Raman, Mantle alijifunza kwamba ma-Buddha walifanya mazoezi mengi magumu yaliyowajenga kuwa watu wa nidhamu ya hali ya juu. Watu hawa walitumia kanuni ya nidhamu ya mazoezi yao ya mwili katika maisha yao ya kila siku. Moja wapo ya maeneo hayo muhimu ni muda. Ma-Buddha waliuchukulia muda kama raslimali adimu na walikuwa makini kutazama vile walivyoutumia. Waliamini mafanikio katika maisha yanaanza na uwezo wa kuudhibiti muda. Muda unakwenda. Saa zinakimbia. Kadri dakika zinavyoyoma ndivyo muda wetu wa kuishi hapa duniani unavyozidi kupungua. Hiyo ni sababu tosha ya kutufanya tutumie muda kwa nidhamu ya hali ya juu tukijua kila dakika inayopotea hairudi tena. Kwa kutambua umuhimu wa muda, jenga tabia ya kutumia dakika 15 usiku kupangilia siku inayofuata. Lakini pia, tumia saa moja siku ya Jumapili, kupangilia juma linaloanza. Ukishaweza kupangilia muda wako, jifunze tabia ya kuwazuia watu wengine kuchezea muda wako. Sema hapana kwa shughuli zisizoendana na majukumu yako. Ishi kama vile una siku moja tu iliyobaki kisha jiulize, “Kama ningekuwa na siku moja tu ya kuishi, hiki ndicho ambacho ningeweza kukifanya?”
Nguzo ya Tano: Furaha ya Kweli Inapatikana kwa Kuwatumikia Wengine na Kuishi Sasa
Nguzo ya tano, kwa mujibu wa Raman, mwalimu wa Mantle, ni kwamba furaha ya kweli haiji kwa kuitafuta bali kwa kuwatumikia wengine. Kuna umuhimu wa kuwa mkarimu mwenye huruma kwa wengine, tabia ambayo, hatimaye itakurudishia matunda wewe mwenyewe. Kila siku asubuhi anza siku kwa kufikiri ufanye nini kwa ajili ya wengine na namna unavyoweza kugusa maisha ya watu wanaokuzunguka. Hili linawezekana kwa kufanya vitu ambavyo wakati mwingine vinaonekana ni vidogo vidogo kama kumpongea mtu kwa kizuri alichofanya, kumsaidia rafiki kwenye shida yake, na kuonesha upendo kwa familia yako. Unapoishi maisha yanayoongeza furaha kwa mwingine, kwa hakika unajiongezea mwenyewe kwenye furushi lako la furaha. Kadhalika, maisha ni sasa. Hatuishi kesho wala jana. Tunaishi leo na sasa hivi. Unapoishi jana, unaweza kujikuta unatumia muda mwingi kujutia au kufurahia mambo yasiyo na uhusiano na yale unayotakiwa kuyafanya leo. Lakini pia unapoishi kesho, maana yake unatumia muda mwingi kupanga mipango inayoweza kukusahaulisha maisha ya leo. Ishi maisha ya leo ukitambua kwamba furaha kamwe haikungoji. Furaha kuhutani nayo mwisho wa safari bali safari yenyewe ndiyo furaha. Kadri tunavyosafiri kwenye safari ya maisha, ndivyo tunavyokutana na matukio yanayofanya maisha yetu yawe ya amani na furaha zaidi. Kadri tunavyosafiri ndivyo tunavyojawa na shukrani kwa vitu kama afya njema tuliyonayo, familia zetu, kazi tulizonazo, vipaji tulivyonavyo, na hata vitu vidogo vidogo kama sauti za ndege tunazozisikia kila siku alfajiri, machweo ya jua, nyota za angani usiku, na hata mawimbi ya bahari tunapokuwa ufukweni. Hakuna kilicho muhimu kama wakati uliopo na maisha tunayoyaishi sasa. Mantile, mhusika wa kitabu hiki, aliporudi kwa rafiki zake, aliwaeleza nguzo hizi. Kuanzia hapo, alianza kuishi maisha ya tofauti, rahisi, yenye utoshelevu. Ukijifunza hilo, utaishi maisha yasiyo na msukumo wa nje wa kuwapendeza watu, wala kuumia kwamba mipango uliyonayo haijafanikiwa.