Jifunze Lugha Tano za Mapenzi

Changamoto za Kudumisha Hisia za Mapenzi

Kila mtu mwenye afya njema anaweza kuanzisha mapenzi. Kwa kawaida, mapenzi yanapoanza, msisimuko huwa ni mkubwa. Ugumu, hata hivyo, ni kuendeleza hisia za mapenzi kwa muda mrefu. Kuendelea kumpenda mtu unayempenda sasa inaweza kuwa moja ya kazi ngumu sana. Si ajabu watu wengi waliooa au kuolewa huishi maisha ya upweke sana wakishindwa kuelewa kitu gani kimeondoa msisimko uliokuwepo wakati mapenzi yao yanaanza. Ndio maana si wengi hudumu kwenye uhusiano ya uchumba kwa muda mrefu. Ndio maana ndoa nyingi huvunjika. Kudumisha penzi ni kazi ngumu inayohitaji kujitoa na kujituma.

Mabadiliko Katika Uhusiano wa Kimapenzi

Gary Chapman, katika kitabu chake cha “The 5 Love Languages: Secret to Love that Lasts” anatoa mapendekezo yanayoweza kuwasaidia wapenzi na wenzi wanaotaka kudumisha mapenzi yao. Niliposoma kitabu hiki wiki hii nilipata mafunzo makubwa matatu makubwa. Kwanza, wapenzi lazima wafahamu kuwa uhusiano wa kimapenzi hubadilika kadri mnavyokuwa pamoja.  Msipokuwa na jitihada za kuwasiliana, uwezekano wa kuendelea kupendana unakuwa mdogo.

Hisia za Awali za Mapenzi Hazidumu

Usitegemee hisia ulizokuwa nazo siku ya kwanza unakutana na mpenzi wako zitadumu. Ile hali ya kukosa usingizi, kumfikiria mwenzako kila dakika, kujisikia kumkosa mwenzako unapokuwa mbali naye, huwa haidumu sana. Baada ya miaka miwili, hisia hizi zinaweza kupotea. Ili kuhuisha hisia hizi, una haja ya kufanya juhudi za kumwelewa mwenzako anataka nini na ufanye nini ajisikie kupendwa. Juhudi hizi ndizo zitakuwezesha kuelewa lugha ya mapenzi anayoielewa zaidi mwenzako.

Kila Mtu Ana Lugha Yake ya Mapenzi

Somo la pili nililojifunza kwenye kitabu hiki ni kwamba, kila mtu ana lugha yake ya mapenzi. Usipoielewa lugha ya mwenzako utakuwa kama mtu anayezungumza ki-Pare kwa mtu anayesikia ki-Nyakyusa. Hamtaelewana kwa sababu unachokifanya hakieleweki kwa lugha ya unayemfanyia.   Gary Chapman anaeleza lugha tano kubwa za mapenzi. Kila lugha ameipa sura inayojitegemea. Lugha ya kwanza, ni maneno yanayotambua alichofanya mwenzako. Kuna watu hawawezi kujisikia kupendwa kama hawajasifiwa na kupongezwa. Kama ni mwanamke, anatamani kuambiwa alivyo mzuri, alivyoumbika, anavyojituma kulea watoto, kupika chakula kizuri na hata kutunza nyumba. Kama ni mwanamume, anatamani kusikia mke wake akimsifia kwa bidii yake kazini, anavyotunza familia, anavyofanya majukumu yake kama mwanamume. Kama mpenzi wako anazungumza lugha hii, usiache kumtambua kile anachokifanya au vile alivyo.

Lugha ya Pili: Muda wa Pamoja

Lugha ya pili ni kupata muda wa kuwa pamoja. Kuna watu namna pekee ya kuwafanya wajisikie kupendwa ni kukaa nao. Hawa wanatamani mkiwa nyumbani usifanye kitu kingine chochote zaidi ya kuzungumza, kufanya vitu pamoja, kutoka kwenda mahali pamoja. Unapokuwa na kazi nyingi ukaweza muda wako mwingi kazini, wanajisikia kukosa kitu muhimu hata kama unawasifia kwa kutumia lugha ya kwanza. Mara ngapi umekaa na mpenzi wako ukaweka simu pembeni na kumsikiliza bila kuangalia televisheni au kushika shika vitu vingine vinavyoingilia uzingativu wako? Kama mpenzi wako anaongea lugha hii, jitahidi kutengeneza ratiba ya kuwa na muda naye.

Lugha ya Tatu: Zawadi

Lugha ya tatu ni zawadi. Mlipokuwa wachumba mlipeana zawadi. Wakati mwingine hamkupeana vitu vikubwa. Pipi au chocolate ilitosha kuonesha kuwa mnapendana. Kwa nini siku hizi hamfanyi hivyo? Kuna watu zawadi zinawagusa sana. Hawa wanachukulia zawadi kama alama ya hisia ulizonazo kwao. Unapomletea mwenzako zawadi unamwambia kuwa huko ulikokuwa ulikuwa unamfikiria. Hisia kama hizi zinaongeza mapenzi kwako. Huhitaji kuwa na fedha nyingi kuzungumza lugha hii. Kama mwenzako anapenda zawadi, jifunze kurudi nyumbani na kitu kidogo kitakachomfanya ajisikie kupendwa.

Lugha ya Nne: Kuhudumiwa

Lugha ya nne ni kuhudumiwa. Kuna watu wanatafsiri mapenzi kama kumsaidia kufanya vitu fulani nyumbani. Unapomhudumia anajisikia vizuri. Kwa mtu kama huyu, anategemea unapokuwa nyumbani umsaidie kazi za ndani. Usibaki umelala kwenye kochi unaangalia taarifa ya habari wakati taa ya bafuni imeungua. Usimke bila kutandika kitanda kwa matarajio kuwa mwenzako atafanya. Watu wanaozungumza lugha hii wanatarajia utafanya kitu kuwasaidia. Kama wewe ni mwanamume, saidia kupiga pasi mara moja moja, mwandalie mke wako chai ya asubuhi mara moja moja, wasaidie watoto kufanya ‘homework’ na vitu kama hivi. Unapofanya hivi unamfanya mke wako ajisikie kupendwa.

Lugha ya Tano: Kuguswa

Lugha ya tano na mwisho kwa mujibu wa Gary Chapman ni kuguswa. Tangu tukiwa watoto tunapendwa kuguswa. Kisaikolojia unapoguswa unajisikia karibu zaidi na aliyekugusa. Hulka hii tunakuwa nayo hata tunapokuwa watu wazima. Tunapokuwa na mtu tumpendaye, tunafurahia kushikwa mikono, kukumbatiwa, kutomaswa, kubebwa na hata kufanya mapenzi. Ingawa hulka hii iko kwa binadamu wengi, wapo wenzetu hii ndiyo lugha inayokuwa na nguvu zaidi kwao. Kama mwenzako anaelewa zaidi lugha hii, jitahidi kumshika mkono mnapotembea, mkumbatie mara kwa mara, unapozungumza naye mguse. Lugha hii ya kuguswa ndiyo anayoielewa zaidi.

Haitoshi Kuelewa Lugha Yako Pekee

Somo la tatu nililolipata kwenye kitabu hiki, ni kwamba haitoshi tu kuelewa lugha yako ya mapenzi. Lazima kuelewa mwenzako anasikia lugha ipi zaidi katika hizo tano. Haitoshi kuelewa lugha ya mwenzako, msaidie kuelewa lugha yake. Ili hili liwezekane, mnalazimika kuwa karibu na kuzungumza kadri inavyowezekana. Wakati mwingine inakuwa rahisi kuelewa lugha zenu za mapenzi kwa kujifunza kile kilichofanya mahusiano yaliyopita. Maumivu mliyoyapata kwa watu wengine yanaweza kuwasaidia kujitambua vizuri zaidi. Pia, ni vizuri kutazama familia mlizotoka. Familia zina nguvu kubwa ya kututengenezea lugha tunazozielewa vizuri zaidi. Ukishaelewa lugha yako, zungumza na mwenzako. Kwa pamoja, itakuwa rahisi kufikia matarajio yenu bila kubahatisha.

Pitio la kitabu hiki limeandikwa na Christian Bwaya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa LEARNING Inspire® TANZANIA.  Unaweza kuwasiliana naye kwa e-mail: bwaya@learninginspire.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *