The 7 Habits of Highly Effective People

Ukitaka kuwa mtu makini shughulikia maeneo saba

Sote tunataka kuwa watu makini. Tungependa tuaminike, tuwe na malengo lakini pia tuweze kusimamia kile tunachokiamini. Kitabu cha ‘The 7 Habits of Highly Effective People’ kilichoandikwa na Stephen R. Covey kinaeleza tabia saba zinazoleta umakini.  Kitabu hiki kinaanza kwa maelezo ya namna watu waliofanikiwa walivyopambana kujenga umakini uliowasaidia kustawisha uhusiano na watu wengine. Kwa kusoma zaidi ya maandiko mengi yanayohusiana na mafanikio tangu enzi za kale, Covey anabainisha namna tafsiri ya mafanikio ilivyobadilika miaka hadi miaka.

Miaka ya kale, kwa mfano, mafanikio yalichukuliwa kama uwezo wa kujenga tunu muhimu katika maisha kama vile uaminifu, unyenyekevu, uadilifu, ujasiri, kiasi na kutenda haki. Lakini kwenye miaka ya 1920, Covey anafikiri, watu walianza kuyatazama mafanikio kwa mtazamo wa nje, yaani heshima mbele za watu, mtazamo anaokuwa nao mtu sambamba na tabia zake. Mitazamo kama hiyo imewafanya watu watamani kupita ‘njia ya mkato’ kufikia mafanikio. Covey anaamini tukitaka kubadilika, lazima tukubali kupitia kwenye mageuzi ya mtazamo na hivyo kuwa tayari kubadilika kuanzia ndani. Je, hilo linawezekanaje? Hapa ninakuletea tabia saba anazopendekeza Covey.

Uwajibikaji

Umakini unaanza na tabia ya kuwajibika. Mtu anayewajibika halalamiki, harushi lawama kwa wengine, hajihurumii kwa sababu anaamini anao uwezo wa kusababisha vitu vikatokea. Covey anasema kuwajibika kunatufanya tuwe na uwezo wa kujikagua, kujitathmini na kuamua vile unavyotaka mambo yaende kwa sababu unaelewa kuwa mustakabali wako unao mikononi mwako mwenyewe. Kinyume na kuwajibika na kuchukua hatua, ni tabia ya kujiona kama mhanga wa mambo yanayotokea hali inayojenga tabia ya kusubiri kupambana na matokeo badala ya kupambana kuleta matokeo.

Kuuona mwisho kabla ya kuanza

Umakini unaanza kwa tabia ya kuona unakoelekea kabla hujaanza safari. Mtu makini haendi asikokujua. Covey anasema lazima uone matokeo ya kile unachokifanya kabla hujakianza. Maana yake lazima uwe na uwezo mkubwa wa kuona yasiyoonekana. Hiyo ndiyo dira ya mafanikio yako. Covey anashauri kwamba kwa kila tunachotaka kukifanya lazima tuanze kwa kujiridhisha na matokeo yake kwanza. Tufanye kama anavyofanya mbunifu wa majengo. Ufahamu wa mbunifu mzuri unaliona jengo lisilokuwepo. Uwezo huo unarahisisha kujua namna ya kujipanga vizuri kuhusu gharama na mahitaji mengine kabla shughuli ya ujenzi haijaanza. Kabla hujaanza biashara, uone mwisho wake. Kiongozi mzuri huona kesho akiwa leo. Mzazi mzuri huona tabia za watoto wake wakiwa watu wazima leo wakiwa watoto. Kabla hatujaanza kufanyia kazi malengo yetu, lazima kuona yanatuelekeza wapi. Kwa kufanya hivyo utavibaini vikwazo kabla havijatokea na hivyo utajipanga vizuri namna ya kukabiliana navyo.  

Kubaini vipaumbele

Umakini pia unategemea uwezo wetu wa kubaini kipi kianze na kipi kisubiri. Huwezi kuwa mtu makini unayefanya kila kitu. Lazima uwe na nidhamu ya kujua vipaumbele vyako. Shughuli unazozifanya kila siku lazima ziendane na vipaumbele ulivyonavyo.  Huwezi kutimiza malengo unayoyaona mbele yako kama hujui kupanga vyema vipaumbele vyako. Ili uwe na vipaumbele lazima ujenge nia ya dhati ya kuachana na baadhi ya mambo yasiyoendana na malengo yako. Covey anatuonesha makundi manne ya shughuli tunazokutana nazo kila siku ambayo ni mambo muhimu na ya dharura; mambo muhimu lakini si ya dharura, mambo yasiyo muhimu lakini ya dharura na yale yasiyo muhimu lakini pia si ya dharura. Mtu makini hutumia muda wake kufanya mambo muhimu lakini yasiyo ya dharura. Kwa kufanya hivyo anajikuta akiwa na muda wa kutosha kufanya vitu kwa umakini na ufanisi kuliko mwezake anayezima moto kwa kufanya mambo ya dharura muda wote.

Usipende kushinda kila kitu

Mafanikio yako yanategemea uhusiano wako na watu. Lazima kuangalia namna unavyoishi na watu bila kujeruhi hisia zao kama kweli unataka kwenda mbele. Dhambi kubwa tunayoifanya ni kupenda kushinda wakati mwingine kwa gharama ya kuwaumiza watu. Huwezi kufanikiwa kwa mtindo huu. Covey anashauri kutokuweka kipaumbele kwenye kushinda na badala yake shinda moyo wa mwenzako. Kwamba si lazima uonekane uko sahihi muda wote. Kuna nyakati unaweza kukubali kuonekana hauko sahihi kwa sababu tu usingependa kumpoteza ndugu yako.

Kuelewa kabla hujataka kueleweka

Kabla hujatoa ushauri kwa mtu, hujamwambia afanye nini kutatua matatizo yake, lazima kwanza ujifunze kuelewa anachokipitia. Huu ndio umakini. Usipende kuamini unajua kabla hujamsikiliza kwa makini mwenzako. Kila mtu anaelewa mambo kwa mtazamo tofauti. Unachoona wewe sicho anachoona mwenzako. Usiwe mwepesi kufikiri kwa niaba ya mwenzako. Mpe nafasi ya kukueleza na wewe jipe muda wa kusikiliza na kuelewa. Bahati mbaya huwezi kusikiliza kama hujaamua kubadili mtazamo wako. Unapokuwa kwenye mazungumzo acha kufanya vitu vingine. Sikiliza kinachosemwa na mwenzako.

Kufungua milango ya kujifunza

Huwezi kuwa mtu makini kama hukubali mawazo mapya. Lazima kuwa tayari kusikiliza mitazamo mipya hata kama wakati mwingine hukubaliani nayo. Waruhusu watu kukuambia yale usiyotaka kuyasikia. Fanya kazi na watu wasiofikiri kama wewe. Hata adui anaweza kuwa mtu wa maana kuliko rafiki ukijua namna ya kuishi naye. Covey anatushauri kujifunza kukubali tofauti zinazokuwepo kwa watu. Katika kila jalala kuna chema. Usiwe mtu wa kuona mabaya pekee. Tukiliweza hilo, Covey anasema tabia ya saba itakuwa rahisi: Kuhuisha nafsi zetu kadri inavyowezekana. Kujipa muda wa kutafakari, kupumzika, kula vizuri, kufanya mazoezi, kusikiliza muziki unaoliwaza, kushiriki kazi za hisani na kujijenga kiroho.

Pitio hili la kitabu limeandikwa na Christian Bwaya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa LEARNING Inspire® TANZANIA.  Unaweza kuwasiliana naye kwa e-mail: bwaya@learninginspire.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *